Kimya cha William Ruto Kinaashiria Anaidhinisha Visa vya Utekaji Nyara, Gachagua Asema
Rigathi Gachagua ameungana na umma kukashifu visa vya utekaji nyara vilivyoshuhudiwa nchini siku za hivi karibuni
Naibu rais huyo wa zamani alipuuzilia mbali taarifa ya Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) ya kuwatenga maafisa kutokana na kutoweka kwa raia
Alidai kuwa dalili zote zinaonyesha kuhusika kwa polisi katika shughuli hizo za kikatili, na hivyo akamkashifu Rais William Ruto kwa kukaa kimya
Aliyekuwa naibu wa rais Rigathi Gachagua ametilia mkazo visa vya utekaji nyara wa raia huku akilaumu hali ya ulegevu katika kuwalinda wakenya.
Aliyekuwa naibu wa rais Rigathi Gachagua alimkabili bosi wake wa zamani kuhusu kunyamazisha utekaji nyara unaoendelea. Picha: Simon Maina.
Chanzo: Twitter
Naibu rais wa zamani alibainisha kuwa vitendo vya kikatili dhidi ya raia wanaokosoa serikali vinaashiria kuwa vyombo vya usalama vimeshindwa kutekeleza majukumu yao ya kuwalinda wananchi.
Akizungumza na wanahabari kutoka nyumbani kwake Nyeri Ijumaa, Desemba 27, Gachagua alidai kwa hisia kali kuwa ukimya wa Rais William Ruto unamaanisha kushiriki kwake kwa njia isiyo ya moja kwa moja katika vitendo hivyo vya utekaji, akimtaka awajibike kikamilifu.
"Lazima awajibike kikamilifu na kushughulikia uvunjaji huu wa haki mara moja. Kubaki kimya au kutofanya chochote kunaashiria kuwa vitendo hivi vinafanywa kwa ufahamu na idhini yake. Haiwezekani kupuuza kuwa kiungo pekee kati ya wahanga ni ukosoaji wao kwa Rais na serikali yake," alisema Gachagua.
Aidha, alidai kuwa anajua mtandao unaoendesha utekwaji huo.
Kulingana na Gachagua, kitengo maalum kilichoundwa kufuatilia wakosoaji kinafanya kazi kutoka jengo fulani jijini Nairobi na kinaongozwa na afisa wa ngazi ya juu mbali na Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja.
Aliapa kufichua walioko nyuma ya mtandao huo endapo kitengo hicho hakitasambaratishwa.
Kwa Nini Gachagua Anamtaka IG Kanja Kujiuzulu
Gachagua aliendelea kumshinikiza Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja na mkurugenzi mkuu wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) Mohamed Amin kujiuzulu kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao.
Alisema wawili hao wameshindwa kuchukua hatua huku Wakenya wakihatarisha usalama wao kwa kukosoa serikali.
Aidha, aliendeleza mashambulizi yake dhidi ya mkurugenzi mkuu wa Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi (NIS), Noordin Haji, akimtaka pia kujiuzulu kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake ya kiraia.
Read ENGLISH VERSION
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia [email protected] au WhatsApp: 0732482690.
Chanzo: TUKO.co.ke