Albert Ojwang: IG Douglas Kanja Afichua Ujumbe Alioandika Marehemu Bloga Kuhusu DIG Lagat Kwenye X

Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja aliieleza Seneti kwamba kukamatwa kwa Albert Ojwang' kulitokana na chapisho kwenye mtandao wa X lililomtuhumu Naibu Inspekta Jenerali Eliud Lagat kwa kupandikiza maafisa waaminifu ili kudhibiti mapato ya polisi na ujasusi

Kanja alisema kuwa chapisho jingine lilimhusisha Lagat pamoja na Kamanda wa Nairobi Joseph Chirchir kwenye mpango wa biashara ya mali isiyohamishika ya mamilioni ya dola huko Dubai, na kumtaja Lagat kama "afisa wa polisi wa mafia."

Alithibitisha kuwa DIG Lagat aliwasilisha malalamiko rasmi Jumatano, Juni 4, hatua iliyochochea uchunguzi wa uhalifu wa mtandaoni ulioongozwa na Kitengo cha Uhalifu Mkubwa

Polisi walifuatilia akaunti ya X hadi kwa Ojwang? kupitia uchunguzi wa kidijitali, ambapo mshukiwa mwenza Kevin Moinde alimtaja kama mmoja wa wachangiaji wanne wa machapisho hayo

Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja amefichua chapisho maalum la mitandao ya kijamii lililoanzisha mlolongo wa matukio yaliyopelekea kukamatwa na kufariki kwa bloga Albert Ojwang'.

IG Douglas Kanja anazungumza mbele ya seneti kuhusu kifo cha Ojwang. Picha: Mzalendo.

Chanzo: Twitter

Chapisho hilo, lililoshirikiwa kwenye akaunti ya X ya Ojwang?, linadaiwa kuwa na madai mazito ya ufisadi dhidi ya Naibu Inspekta Jenerali (DIG) Eliud Lagat.

Akizungumza mbele ya Seneti siku ya Jumanne, Juni 10, Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja alisema kuwa chapisho hilo lilidai kuwa Lagat alipanga operesheni ya kuweka maafisa wake wa kuaminika kwenye nafasi muhimu za uongozi ndani ya huduma ya polisi.

?Haswa, taarifa hiyo ilidai kuwa Bw. Eliud Lagat aliweka kimakusudi maafisa wake waaminifu kusimamia madawati ya DCI, vitabu vya matukio (occurrence book), na fomu za trafiki ili kudhibiti mapato na mtiririko wa taarifa za kijasusi,? Kanja aliambia Seneti.

Alisema kuwa madai hayo yaliibua wasiwasi mkubwa kwa umma na yalistahili kuchunguzwa chini ya Sheria ya Matumizi Mabaya ya Kompyuta na Uhalifu wa Mtandaoni ya 2018.

Aidha, Kanja alifichua kuwa chapisho lingine lilimhusisha Lagat na Kamanda wa Nairobi, Joseph Chirchir, likiwahusisha na dili kubwa ya mali isiyohamishika (real estate).

Chapisho hilo lilijumuisha picha ya Lagat pamoja na maandishi yaliyodai kuwa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) ilikuwa ikimchunguza.

?EACC inachunguza afisa wa juu baada ya kununua nyumba ya dola milioni 2.6 Dubai,? liliandika chapisho hilo likiwa na picha ya DIG na maneno ?Eliud Lagat ? Mafia Police?, kama alivyonukuliwa Kanja.

Kulingana na Kanja, machapisho hayo yalikuwa ya kuchafua jina, yasiyo na ushahidi, na yenye hatari, hasa ikizingatiwa kuwa akaunti ya Ojwang? ilikuwa na wafuasi 13,400.

DIG Lagat aliwasilisha rasmi malalamiko kwa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) mnamo Juni 4, na uchunguzi wa uhalifu wa mtandaoni ukaanzishwa.

Polisi walimnasa vipi Ojwang??

Kikosi cha uchunguzi ya DCI kilichoongozwa na Mkuu wa Polisi Mwandamizi, Hillary Mutai, kiliteuliwa mara moja.

Wachunguzi walitafuta usaidizi kutoka kwa EACC ili kuthibitisha kama Lagat alikuwa anachunguzwa, na vilevile waliwasiliana na Mamlaka ya Mawasiliano ya Kenya (CA) kwa ajili ya uchunguzi wa kidijitali.

Ifikapo Alhamisi, Juni 5, EACC ilithibitisha kwa maandishi kuwa Lagat hakuwa anachunguzwa kwa madai yoyote ya ufisadi.

Wakati huo huo, CA ilithibitisha kuwa akaunti ya X iliyohusika ilikuwa imesambaza maudhui yanayofanana kupitia mtandao wa watumiaji.

Uchunguzi huo wa kidijitali uliwaongoza polisi hadi kwa Kevin Moinde, ambaye alikamatwa katika kaunti ya Kisii.

Wakati wa mahojiano, Moinde aliwataja watu wengine wanne wakiwemo Ojwang?, Dorcas Mawia, Douglas Marigiri na Peter Mbugua kama wachangiaji wa machapisho hayo.

?Kevin alitoa taarifa na kufichua ushiriki wa watu wanne wengine pamoja na kufichua majina ya akaunti zao za X,? Kanja alieleza.

Wajackoyah amkemea DIG Lagat

Kiongozi wa chama cha Roots, George Wajackoyah, awali alitoa wito wa kusimamishwa kazi mara moja kwa Lagat, akitilia shaka ni kwa nini Lagat ? ambaye ndiye mlalamikaji ? aliruhusiwa kusimama karibu na IG Kanja katika mkutano wa polisi.

Alisema kuwa uwepo wa Lagat unaweza kuathiri uchunguzi, na alisisitiza kuwa maafisa wote waliomhusisha Ojwang? katika kukamatwa kwao watambuliwe na wasimamishwe kazi.

Wajackoyah pia alitaja mifano ya kimataifa akihoji kama Ojwang? alielezwa haki zake wakati wa kukamatwa.

Read ENGLISH VERSION

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia [email protected] au WhatsApp: 0732482690.

Chanzo: TUKO.co.ke