Albert Ojwang: CCTV Katika Ofisi ya OCS wa Central Zilivurugwa, IPOA Yaeleza Seneti

Naibu Mwenyekiti wa Mamlaka Huru ya Kutathmini Utendakazi wa Polisi (IPOA), Ann Wanjiku, alihudhuria kikao cha Seneti kuhusiana na kifo cha bloga Albert Ojwang

Wanjiku alieleza matokeo ya awali ya uchunguzi wa IPOA, yakiwemo madai ya kuvurugwa kwa mfumo wa CCTV katika Kituo cha Polisi cha Central

Maseneta walimtaka Inspekta Mkuu wa Polisi, Douglas Kanja, kutoa majibu kuhusu mtu aliyeharibu ushahidi wa CCTV

Nairobi - Mamlaka Huru ya Kutathmini Utendajikazi wa Polisi (IPOA) imeshiriki matokeo ya awali ya uchunguzi wake kuhusu mazingira yaliyosababisha kifo cha bloga Albert Ojwang.

IPOA CCTV katika kituo cha Central iliingiliwa. Picha: Albert Ojwang/NPS/Getty Images.

Chanzo: Facebook

Akizungumza mbele ya Seneti siku ya Jumatano, Juni 11, Naibu Mwenyekiti wa IPOA, Ann Wanjiku, alifichua kuwa wamepata ushahidi unaopingana na ripoti ya awali ya polisi iliyodai kuwa Ojwang alijiua.

Kulingana na Wanjiku, kikosi cha uchunguzi cha IPOA kilibaini kuwa mfumo wa CCTV katika ofisi ya OCS wa Kituo cha Polisi cha Central ulikuwa umechezewa.

"Mifumo ya CCTV iliyoko katika ofisi ya OCS wa Kituo cha Polisi cha Central imeingiliwa. Uchunguzi wa awali kuhusu kifo cha Albert Ojwang akiwa korokoroni unapinga madai kuwa alijiua," alisema Wanjiku.

Ufunuo huo ulisababisha hasira miongoni mwa maseneta, wengi wao wakitaka kujua ni nani aliyeharibu ushahidi wa CCTV katika Kituo cha Polisi cha Central.

Seneta wa Nyamira, Okong?o Omogeni, aliomba DCI kutoa video za CCTV zinazoonyesha safari ya Ojwang kutoka Homa Bay hadi Central Police Station:

"Ninaamini mna kamera za CCTV. Kama tunataka kufuatilia matukio kabla ya kijana huyu kufikishwa Central Police, je, tunaweza kuona video hizo? Hili litatusaidia kujua kama aliwasili akiwa hai au la," alisema Omogeni.

Seneta wa Kitui, Enock Wambua, naye alisema:

"IG Kanja, ni nani aliyeharibu video za CCTV usiku ambao Albert aliuawa? Na huwezi kutuambia hujui kwa sababu hilo litakuwa tatizo kubwa."

Je, Albert Ojwang alifika salama Nairobi?

Wakati huo huo, Mkuu wa Polisi nchini, Douglas Kanja, aliambia Seneti kuwa bloga huyo alifika salama Nairobi kutoka Homa Bay, ambako alikamatwa na maafisa wa DCI.

Kulingana na Kanja:

Ojwang alifikishwa Kituo cha Polisi cha Central na OCS alihakikisha kuwa alikuwa na hali nzuri ya kiafya kabla ya kufungwa.

Alimpigia mke wake simu saa 3:24 usiku, dakika 11 kabla ya kufungwa, kuthibitisha kuwa alikuwa amewasili Nairobi.

Polisi walieleza kuwa walipofika Narok, walisimama kupata vinywaji, ambapo Ojwang alipatiwa maji, soda, na biskuti.

Albert Ojwang alifariki katika Kituo cha Polisi cha Central. Picha: Albert Ojwang.

Chanzo: Twitter

Unachopaswa kujua kuhusu kifo cha Albert Ojwang?

IPOA imefichua majina ya maafisa wa DCI waliomkamata Albert Omondi Ojwang huko Homa Bay.

IG Kanja aliiambia Seneti kuwa kisa cha kukamatwa kwa Ojwang kilitokana na chapisho mtandaoni kilichomtuhumu Naibu IG Eliud Langat kwa kupandikiza maafisa waaminifu ili kudhibiti mapato na ujasusi wa polisi.

Jumanne, Juni 10, mtaalamu wa upasuaji Bernard Midia alifichua kuwa Ojwang alikufa kutokana na majeraha ya kichwa na kukandamizwa shingoni.

Read ENGLISH VERSION

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia [email protected] au WhatsApp: 0732482690.

Chanzo: TUKO.co.ke