Mkewe Albert Ojwang Asema Mwalimu Aliyeuawa Alikuwa na Ndoto Kubwa kwa Familia

Albert Ojwang, mwalimu mwenye umri wa miaka 31, mume na baba wa mtoto mmoja, alifariki akiwa mikononi mwa polisi, jambo lililozua ghadhabu miongoni mwa umma

Alikamatwa Ijumaa, Juni 6, wakati akila chakula cha mchana kwenye boma la babake katika kijiji cha Kakoth, Kabondo Kasipul, kaunti ya Homa Bay

Mjane wake, Nevinina Onyango, ambaye walikuwa wameoana hivi majuzi, aliomboleza kifo chake huku akisimulia ndoto walizokuwa nazo kwa ajili ya familia yao

Kifo cha Albert Ojwang kimeibua hasira kote nchini, huku Wakenya wakitaka haki itendeke kwa familia yake.

Mkewe Albert Ojwang aomboleza mume aliyeuawa. Picha: Albert Ojwang/Daily Nation.

Chanzo: Facebook

Bloga na mwalimu mwenye umri wa miaka 31 alikamatwa akiwa anakula chakula cha mchana katika boma la babake huko Kabondo Kasipul, kaunti ya Homa Bay, siku ya Ijumaa, Juni 6, kwa madai ya kumkosea heshima afisa mwandamizi wa polisi.

Baadaye, Albert alihamishiwa hadi Kituo Kikuu cha Polisi cha Nairobi, ambako alizuiliwa kabla ya kufariki kwa hali ya kutatanisha siku ya Jumapili, Juni 8.

Awali, polisi walitoa taarifa wakidai kwamba baba huyo wa mtoto mmoja alijigonga kichwa ukutani akiwa seli, akapatikana akiwa amepoteza fahamu na kupelekwa katika Hospitali ya Mbagathi, ambako alitangazwa kufariki alipowasili.

Hata hivyo, uchunguzi wa maiti uliofanywa Jumanne, Juni 10, ulibaini kuwa Albert alifariki kutokana na majeraha mabaya kichwani yaliyosababishwa na kupigwa na kifaa butu, pamoja na majeraha mengine mengi yaliyotokana na kichapo.

Ufunuo huu uliamsha hasira zaidi, huku familia, wananchi na baadhi ya viongozi wakitaka uchunguzi wa haraka na haki kutendeka kwa wahusika kuadhibiwa.

Mjane wa Albert Ojwang Nevinina Onyango anamuomboleza mume wake aliyefariki akiwa mikononi mwa polisi jijini Nairobi. Picha: Nation Daily.

Chanzo: UGC

Mke wa Albert Ojwang alimhuzunikia vipi?

Kulingana na ripoti ya Ramogi TV, baba wa Albert, Meshack Ojwang, alifichua kuwa mwanawe alikuwa amejitambulisha rasmi kwa familia pamoja na mkewe, Nevinina Onyango, mwezi Aprili mwaka huu, na walikuwa wamejaliwa mtoto mmoja.

Alieleza kuwa Nevinina alikuwa mgeni katika familia, na ndio sababu Albert alisafiri kutoka Voi ambako alikuwa akifanya kazi, kuja kuwa naye nyumbani kwao huku wakijiandaa kuanza maisha mapya.

Nevinina alimuomboleza mumewe kwa huzuni akisema kuwa Albert alikuwa na ndoto kubwa na mipango mikubwa kwa ajili ya familia yao.

Waliagana kwa mara ya mwisho wakila chakula cha mchana pamoja, muda mfupi kabla ya maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kufika nyumbani kwao na kumchukua Albert.

Je, Albert Ojwang alikuwa mtoto pekee?

Katika taarifa nyingine iliyoripotiwa na TUKO.co.ke, babake marehemu, Meshack, alifichua kuwa Albert alikuwa mtoto wake wa pekee.

Baba huyo aliyesononeka alishiriki kwamba hana matumaini tena ya kupata mtoto mwingine, kwa kuwa umri wake umesonga na hata akijaribu, hataweza kumlea hadi kufikia kiwango ambacho Albert alikuwa amefikia.

Meshack alisema kuwa matumaini yake na ya familia nzima yalivunjika baada ya kifo cha mwanawe, na akashinikiza haki itendeke.

Wakenya wafariji mjane wa Albert Ojwang

Mireri Ann Awuor:

?Inahuzunisha sana, lakini Mungu atakuwa pamoja nawe mpenzi, na akutie nguvu na amani kulea malaika wako mdogo.?

Hyda Murungi:

?Moyo wangu unauma, Bwana mfariiji.?

Gerald Githuku:

?Mtu salama pekee kwa sasa Kenya ni yule aliye Kamiti ama Mathare. Sisi wengine tunaweza kutekwa nyara muda wowote. Wacha nisimame niseme.?

Emily Miriga:

?Mungu niweke tu hadi 2027, hili linahuzunisha sana, msichana mdogo hivi tayari amekuwa mjane? Mungu kwa nini? Lakini najua Mungu yupo. Albert usilale bro.?

Read ENGLISH VERSION

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia [email protected] au WhatsApp: 0732482690.

Chanzo: TUKO.co.ke