Justin Muturi Atupa Jiwe kwa Ruto, Ahoji Kuhusu Raila Kupeana Ardhi Ili Kujengwe Nyumba za Bei Nafuu

Aliyekuwa Waziri wa Utumishi wa Umma Justin Muturi alitilia shaka madai ya Rais William Ruto kwamba Raila Odinga alitoa ekari tano za ardhi Kisumu kwa ajili ya makazi ya gharama nafuu

Muturi alishutumu serikali ya Kenya Kwanza kwa kutumia Mpango wa Nyumba za bei nafuu kama sehemu ya mbele ya uporaji

Mwanasheria Mkuu huyo wa zamani alionya kwamba msukumo wa Ruto wa mageuzi ya makazi ni zaidi ya manufaa ya kibinafsi kuliko manufaa ya umma

Aliapa kwamba upinzani utarejesha utajiri ulioibiwa iwapo utachaguliwa mwaka wa 2027, akisema utawala wa Ruto ndio utakuwa mwanzo wa uwajibikaji

Aliyekuwa Waziri wa Utumishi wa Umma Justin Muturi amemwagia maji baridi madai ya Rais William Ruto kwamba kinara wa ODM Raila Odinga alitoa ekari tano za ardhi ya familia yake huko Kisumu kwa ajili ya Mpango wa Nyumba ya Affordable Housing.

Aliyekuwa Waziri wa Utumishi wa Umma Justin Muturi alizidisha ukosoaji wake dhidi ya utawala wa Ruto. Picha: Justin Muturi.

Chanzo: Twitter

Matamshi yake yalijiri siku moja tu baada ya Ruto, alipokuwa akiwahutubia wakazi wa Kisumu, kummiminia Raila sifa kwa kutoa ardhi kuwezesha ujenzi wa nyumba 750 za bei nafuu.

Rais alitaja ishara hiyo kama ishara ya umoja na onyesho la dhamira ya waziri mkuu huyo wa zamani katika kuinua maisha katika eneo hilo.

Mbona Muturi alitilia shaka mchango wa Raila

Wakati wa hafla ya kisiasa katika kaunti ya Machakos mnamo Ijumaa, Mei 30, Muturi alihoji waziwazi uhalisi wa mchango huo.

Muturi alishutumu utawala wa Kenya Kwanza kwa kutumia ajenda ya makazi kama njia ya ufisadi, kunyakua pesa za umma.

Mwanasheria Mkuu huyo wa zamani alidiriki serikali kutangaza hadharani hati miliki ili kuthibitisha mchango unaodaiwa wa Raila.

"Ngoja nikupe onyo dogo, kila unapomsikia William Ruto akisukuma kitu kigumu sana, ujue anatafuta mfuko wake mwenyewe. Unanielewa? Juzi tu, yeye mwenyewe alidai kuwa Raila Odinga alitoa ekari tano kwa serikali. Kweli? Raila alitoa ekari tano? Kisha tuseme hivi kwa William Ruto: kwa vile tunakufahamu, tuonyeshe hati tano hizo," alisema.

Lakini Muturi, ambaye awali aliwahi kuwa Spika wa Bunge la Kitaifa, haununui mradi huo wa nyumba.

Alidokeza kuwa kisa chote kilikuwa kifusi cha ufujaji wa pesa za umma, huku akimnyooshea vidole Naibu Rais Kithure Kindiki kwa madai ya kutorosha nyara hizo.

"Kwa sababu, jinsi watu wengine walivyotuambia, ni pesa hizo za nyumba ambazo Ruto ameanza kupora," Muturi alisema.

Upinzani utamwajibisha vipi Ruto

Mpango wa Nyumba za bei nafuu, sera kuu ya Ruto, umevutia sifa na ukosoaji mkali tangu kuanzishwa kwake.

Muturi hakuishia kupinga shughuli hiyo ya ardhi, na kutoa onyo kali kwa mkuu wa nchi.

Justin Muturi akihutubia mkutano siku zillizopita. Picha: Justin Muturi.

Chanzo: Facebook

Waziri huyo wa zamani aliahidi kwamba utawala wa Ruto utawajibishwa iwapo upinzani utashinda Uchaguzi Mkuu wa 2027.

"Tuko hapa. Hii ndiyo serikali inayokuja, na inakuja kuhakikisha kwamba utajiri wote wa Kenya ambao umeibiwa unarudishwa kwa wananchi. Ni lazima tuweke wazi kabisa: hakuna mtu atakayechaguliwa tena kuiba kutoka kwa Jamhuri ya Kenya na kwamba uwajibikaji lazima uanze na utawala wa Ruto," Muturi alitangaza.

Ni watu wangapi walipewa nyumba huko Mukuru

Mnamo Jumanne, Mei 20, Ruto alikabidhi nyumba 1,080 za bei nafuu kwa wakazi wa Mukuru, mojawapo ya makazi duni makubwa zaidi ya Nairobi.

Alitaja tukio hilo kuwa muhimu zaidi katika safari yake ya kisiasa.

Ruto alisema mpango huo ni sehemu ya mpango mpana wa kukabiliana na hali duni ya maisha, ikiwemo msongamano wa watu, ukosefu wa usalama na ukosefu wa huduma za kimsingi.

Alitangaza kwamba Jengo la New Mukuru Housing Estate hatimaye litakuwa na vitengo 13,248, na kuifanya kuwa eneo kubwa zaidi la maendeleo ya mali isiyohamishika nchini Kenya.

Read ENGLISH VERSION

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia news@tuko.co.ke au WhatsApp: 0732482690.

Chanzo: TUKO.co.ke