Seneta wa Bungoma Asema Liwe Liwalo, Yeye na Natembeya Kitaeleweka Kuanzia Wiki Ijayo: "Washeni TV"

Seneta wa Bungoma, David Wakoli, ametangaza vita vya kisiasa dhidi ya Gavana wa Trans Nzoia, George Natembeya, akisema kuwa atamkabili Seneti ili awajibike kwa uongozi wake

Wakoli alimtuhumu Natembeya kwa unafiki kwa kuandaa mikutano ya hadhara ya kuwakosoa viongozi wengine huku akipuuzia changamoto katika kaunti yake mwenyewe

Kauli hiyo ilijiri baada ya ziara ya Natembeya katika maeneo ya Magharibi mwa Kenya licha ya mashtaka ya ufisadi yanayomkabili, ambapo alisisitiza msimamo wake wa kuikosoa serikali ya Kenya Kwanza

Gavana wa Trans Nzoia, George Natembeya, anatarajiwa kufikishwa mbele ya Kamati ya Kilimo, Uchumi wa Bahari na Mifugo ya Seneti inayoongozwa na Seneta David Wakoli, Alhamisi tarehe 29 Mei.

Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya anatarajiwa kuhojiwa na kamati inayoongozwa na seneta wa Bungoma David Wakoli. Picha: George Natembeya, David Wakoli.

Chanzo: Facebook

Akizungumza katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Cardinal Otunga wakati wa makabidhiano rasmi ya bweni jipya lililojengwa na Taasisi ya Kenya Pipeline Company, Wakoli alimshtumu Natembeya kwa kupotosha umma na kukwepa uwajibikaji.

?Kama mwenyekiti wa kamati, nitahakikisha kuwa Natembeya anawajibika kwa namna anavyoendesha mambo katika Trans Nzoia. Ni wakati wa kupata majibu,? alisema Wakoli.

Aliwataka Wakenya kufuatilia vikao hivyo kupitia runinga.

?Hakikisha runinga zenu zimewashwa. Tazameni jinsi tunavyomhoji. Ikiwa amekosea, lazima awajibike,? aliongeza.

Wakoli pia alitoa kauli tata ya kidini kwa kumlinganisha Natembeya na Barnaba, mhusika wa Biblia aliyeachiliwa huru huku Yesu akisulubiwa.

?Barnaba yuko hapa Trans Nzoia. Ni wakati wetu kumsulubisha na kumwondoa njiani,? alisema Wakoli.

Seneta huyo alimkosoa Natembeya kwa kuzuru maeneo mbalimbali ya Magharibi mwa Kenya na kuandaa mikutano ya kisiasa katika kaunti zingine, akimtuhumu kwa kulaumu wengine badala ya kutatua matatizo katika kaunti yake.

?Viongozi kutoka nje ya Bungoma wanadhani wanaweza kuja, kufanya maandamano, na kutueleza jinsi ya kuendeleza maendeleo, ilhali kaunti zao zimesalia nyuma huku Bungoma ikiendelea,? aliongeza.

Wakoli alitetea utendaji wa serikali ya Bungoma akitaja miradi mikuu ikiwemo ofisi mpya ya uhamiaji kwa urahisi wa huduma, hospitali ya kiwango cha sita, Uwanja wa Ndege wa Matulo, Uwanja wa Kanduyi, mpango wa makazi, na hifadhi ya viwanda.

Alisema miradi hiyo itaongeza uchumi wa Bungoma na kutoa ajira bora kwa wakaazi wa eneo hilo.

Kwa nini Natembeya alikuwa akizuru Magharibi mwa Kenya?

Matamshi ya Wakoli yalitolewa baada ya ziara ya hivi majuzi ya Natembeya katika kaunti za Kakamega, Vihiga na Bungoma.

Gavana huyo alipokelewa kwa shangwe katika ziara hiyo iliyofuata kukamatwa kwake na kufikishwa mahakamani kwa mashtaka ya ufisadi.

Katika hotuba zake za barabarani, Natembeya alisisitiza msimamo wake dhidi ya serikali ya Kenya Kwanza. Alisema kuwa serikali inapaswa kuruhusu maoni tofauti badala ya kuyakandamiza.

Pia alimkosoa Waziri Mkuu wa Baraza la Mawaziri, Musalia Mudavadi, na Spika wa Bunge la Taifa, Moses Wetang?ula, kwa madai ya kuwasaliti watu wa jamii ya Waluhya.

Seneta wa Bungoma alitishia vita dhidi ya gavana wa Trans Nzoia George Natembeya. Picha: David Wakoli.

Chanzo: Facebook

Kwa nini Caleb Amisi alimtetea Natembeya?

Katika taarifa ya awali kwa TUKO.co.ke, Mbunge wa Saboti, Caleb Amisi, aliwalaumu vikali viongozi wa Magharibi mwa Kenya waliosherehekea kukamatwa kwa Natembeya.

Akizungumza katika Kanisa la Kipentekoste la Kitale, Amisi alisema kuwa hatua hiyo ilikuwa isiyo ya kiungwana na usaliti kwa mshikamano wa eneo hilo.

Aliwahimiza viongozi wenzake kusimama na Natembeya bila kujali tofauti za kisiasa, akionya kuwa kukosa kupinga dhuluma leo kunaweza kuleta madhara kwao baadaye.

Amisi, ambaye ni mshirika wa karibu wa gavana huyo, alisema kuwa mashtaka ya ufisadi yanaonekana kuchochewa kisiasa, na kuwataka Wakristo waendelee kumuombea Natembeya.

Read ENGLISH VERSION

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia news@tuko.co.ke au WhatsApp: 0732482690.

Chanzo: TUKO.co.ke