Susan Wangeci: Mumewe Mwanamke Aliyetoweka Baada ya Kufanya Manunuzi Eastleigh Asema Hajapatikana

Joseph Maina alizungumza mara ya mwisho na mkewe aliyepotea, Susan Wangeci Karingi, siku ya mkasa alipoweka tu simu na kutoweka kabisa bila kuacha dalili

Alikuwa anaenda kwenye mkutano wa chama kabla ya kuelekea soko la Eastleigh kununua bidhaa chache kwa ajili ya duka lake lililoko Pipeline

Baada ya kuzungumza na mkewe majira ya saa nane mchana, Maina alisema hakusikia tena kutoka kwa mpenzi wake na mama wa watoto wao wawili

Familia ya mwanamke huyo aliyepotea alipokuwa akitekeleza shughuli zake Eastleigh, kaunti ya Nairobi, hatimaye wamevunja kimya chao.

Joseph Maina (kushoto) afunguka kuhusu kutoweka kwa mkewe, Susan Wangeci (kulia). Picha: Kenya Digital News, Ndungu Nyoro.

Chanzo: Youtube

Susan Wangeci Karingi alitoweka katika mazingira ya kutatanisha alipokuwa akienda kununua bidhaa za kuongeza kwa duka lake lililoko Pipeline.

Kulingana na picha za CCTV, Wangeci mwenye umri wa miaka 47 alionekana mara ya mwisho katika duka moja eneo la Eastleigh akinunua bidhaa kabla ya kutoweka ghafla.

Wangeci alitoweka lini?

Mume wake, Joseph Maina, alisimulia kwa majonzi kuhusu siku ya mwisho aliyomwona mkewe kabla ya kutoweka mnamo Jumatano, Mei 14.

?Siku hiyo ya tukio, Wangeci aliondoka nyumbani saa tatu asubuhi. Alikuwa akielekea kwenye mkutano wa chama katika Kanisa la Kiprotestanti la Afrika Mashariki (PCEA) Pipeline kabla ya kuelekea soko la Eastleigh. Mimi sikuwa naenda kazini siku hiyo, hivyo nilikuwa nyumbani. Nilimpigia simu saa nane mchana kumuuliza kama alikuwa amenunua vitu alivyokusudia na kama alikuwa njiani kurudi nyumbani kwa sababu nguo zilikuwa zimeshaanikwa na zilihitaji kuondolewa?lakini nililazimika kuziondoa mwenyewe,? alieleza Maina.

Maina afichua mkopo wa chama wa mkewe

Maina, baba wa pacha wa kike, alisema hakumpigia simu tena mkewe siku hiyo kwa kuwa alikuwa na hakika angerudi nyumbani kama kawaida.

Hata hivyo, ilipofika jioni na Wangeci hajarudi, alianza kuwa na wasiwasi.

?Niliamua kumpigia simu saa nne usiku, lakini simu yake haikupatikana. Tangu wakati huo, hajajulikana alipo. Siku iliyofuata nilianza kumtafuta katika maduka mbalimbali Eastleigh na kuwauliza wauzaji kama walimwona. Tuliambiwa alionekana na mwanamke mwingine karibu na saa saba mchana, lakini hatujafanikiwa kumtambua mwanamke huyo. Pia tuliambiwa alikuwa na mkopo wa chama, lakini alikuwa analipa vizuri bila matatizo yoyote. Alikuwa mwaminifu na makini katika kulipa deni lake, hakuna rekodi ya kuchelewa,? Maina alisema.

Watoto wa Wangeci waomba arudi nyumbani salama

Maina, ambaye ameishi na Wangeci kwa zaidi ya miaka 20, alisema ndoa yao ilikuwa na amani, na hata walipopishana kimtazamo, walitatua changamoto hizo kwa utulivu.

Aliomba kwa uchungu mkewe arejeshwe salama, akimsihi yeyote anayemshikilia ampatie uhuru wake kwani familia imegubikwa na majonzi.

?Tafadhali mwachieni. Kama kuna shida yoyote, tutashughulikia. Tumejaa hofu. Watoto, ambao wako chuo kikuu, wanaumia sana. Kila siku wanalia wakimuulizia mama yao?atakaporudi au ikiwa atarudi. Wamevunjika moyo kabisa,? alisema Maina.

Mama wa Nakuru alilia baada ya mwili wa mhudumu wa M-Pesa aliyepotea kupatikana

Katika taarifa nyingine, mama wa msichana mmoja aliyekuwa mhudumu wa M-Pesa alizidiwa na majonzi baada ya mwili wa binti yake kupatikana mochari.

Hannah Waithera alitoweka baada ya kutumwa kuweka KSh 250,000 katika akaunti ya benki ya mwajiri wake.

Baada ya kutoweka kwa siku kadhaa, mwili wake ulipatikana mochari, na kusababisha mamake kuangua kilio kwa huzuni.

Read ENGLISH VERSION

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia news@tuko.co.ke au WhatsApp: 0732482690.

Chanzo: TUKO.co.ke