Kalonzo Awatambulisha Wanawe, Mabinti Wakwe Kitui kwa Upendo: "Mama Yao Anatazama Kwa Runinga"

Stephen Kalonzo Musyoka aliwaalika viongozi wakuu wa upinzani, akiwemo Rigathi Gachagua, katika nyumbani kwake kaunti ya Kitui

Mwanasiasa huyo wa upinzani aliwatambulisha wanawe watatu: wawili wameoa na mmoja bado anatafuta mwenza

Mke wa Kalonzo, Pauline, hakuweza kuhudhuria hafla hiyo kkwani ni mgonjwa, lakini alifuatilia matukio kupitia kwa runinga

Kiongozi wa chama cha Wiper, Stephen Kalonzo Musyoka, ametaimbulisha familia yake.

Kalonzo Musyoka akiwa na wanawe Kennedy (kushoto) na Kevin (kulia) pamoja na wakwe zake huko Kitui. Picha: Kalonzo Musyoka.

Chanzo: Twitter

Mwanasiasa huyo aliwaalika wanasiasa wakuu wa upinzani, akiwemo aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, katika boma lake huko Tseikuru, kaunti ya Kitui.

Wakati wa hotuba yake, Kalonzo aliwaalika wanawe jukwaani na kuwafahamisha marafiki zake.

Familia ya Kalonzo Musyoka

Kati ya wanawe watatu, wawili wao tayari wameoa na walikuwa wameambatana na wake zao, huku mmoja akiwa bado hajapata jiko.

Mkewe Kalonzo, Pauline, hakuwepo katika hafla hiyo, na Kalonzo alieleza kuwa alikuwa akifuatilia matukio kwenye runinga.

Pauline amekuwa mgonjwa kwa muda mrefu na hajakuwa hadharani kwa miaka mingi.

Wa kwanza kutambulishwa alikuwa mwanawe Kevin Muasya pamoja na mkewe. Wanandoa hao walifunga pingu za maisha Jumamosi, Mei 10, katika harusi ya kifahari mjini Nakuru.

Harusi hiyo ilihudhuriwa na marafiki wenye ushawishi wa Kalonzo.

"Njoo hapa ili tupigwe picha pamoja. Mama yao anaangalia hafla hii kwa runinga. Tumpigie makofi na tumuombee apate nguvu ya kupona. Huyu anaitwa Kevin Muasya, na hivi majuzi tu alipata mke. Ahsanteni sana," alisema.

Kisha akaendelea kumtambulisha mwanawe mwingine, Kennedy, na mkewe.

"Huyu mwingine anaitwa Kennedy. Yeye ni Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA). Mke wake ni mama wa Pauline. Wana mtoto aitwaye Pauline. Tuwapigie makofi," Kalonzo aliongeza.

Kalonzo kisha aligeukia mwanawe wa mwisho ambaye alionekana kusita kujiunga jukwaani.

"Mailu yuko mahali hapa. Yuko pale. Mailu ni Gen Z. Tafadhali njoo. Yeye ndiye peke yake ambaye bado hana mke. Anatafuta mwenza. Tuwapigie makofi," Kalonzo alisema.

Kalonzo apokea zawadi ya shuka kwa ajili ya mkewe

Miezi michache iliyopita, wakati wa ibada katika eneo la Dagoretti North, mhubiri alimzawadia Kalonzo shuka jeupe ili ampelekee mkewe mgonjwa.

Mhubiri huyo alimwita Kalonzo jukwaani, akampa shuka hiyo na kumuombea Pauline apone, jambo lililomgusa Kalonzo kwa kiasi kikubwa.

Kalonzo alikutana vipi na mkewe?

Kalonzo na Pauline wamekuwa katika ndoa tangu 1985 na wamebarikiwa na watoto wanne wa kupendeza.

Mnamo mwaka wa 2021, mwanasiasa huyo mkongwe alifichua kuwa alikutana kwa mara ya kwanza na Pauline mwaka wa 1972, wakati alikuwa kidato cha pili katika Shule ya Wasichana ya Mlango.

Walikutana katika Mkutano wa Kikristo uliofanyika katika Shule ya Meru, ambapo Kalonzo alikuwa kidato cha tano.

Kalonzo Musyoka akiwa na mkewe Pauline. Picha Kalonzo Musyoka.

Chanzo: UGC

Alivutiwa naye mara moja kutokana na urembo wake, urefu wake, na nywele zake ndefu.

Pauline anaumwa na nini?

Mnamo Julai 2019, kiongozi wa chama cha Wiper alitoa maelezo kuhusu changamoto za kiafya za mkewe, ambazo zimehusisha ziara nyingi hospitalini humu nchini na nje ya nchi tangu mwaka wa 2015.

Inaripotiwa kuwa Pauline amekuwa mgonjwa tangu 2015 kutokana na ugonjwa ambao haukufichuliwa, na wakati mmoja alisafirishwa nje ya nchi kwa matibabu maalum.

Read ENGLISH VERSION

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia news@tuko.co.ke au WhatsApp: 0732482690.

Chanzo: TUKO.co.ke