Taarifa Mpya Zaonyesha Jamaa Mkenya Alifariki Akijaribu Kuwaokoa Marafiki Katika Moto wa UAE

Mwanamume mmoja raia wa Kenya ni miongoni mwa watu watano waliofariki katika ajali ya moto iliyotokea kwenye jengo la ghorofa ya juu katika eneo la Al Nahda huko Sharjah

Kabla ya kifo chake, mtu huyo alijulikana kwa jina la B.K. alikuwa amewaamsha wenzake na kuwaelekeza jinsi ya kuepuka kukosa hewa wakati wa moto

Kwa bahati mbaya, wakati timu za ulinzi wa raia ziliwaokoa wenzake, B.K. alipotea na baadaye alipatikana akiwa amekufa baada ya kujaribu kutoroka moto kwa kutumia kebo

Taarifa mpya zimeibuka kuhusu raia wa Kenya ambaye alikuwa miongoni mwa watu watano waliofariki kwenye ajali ya moto ya mnara wa Al Nahda huko Sharjah Jumapili, Aprili 13.

Mnara wa Al Nahda ukiwaka moto (kulia) na picha ya wazima moto (picha iliyo upande wa kulia kwa kielelezo). Picha: Khaleej Times/Natnan Srisuwan.

Chanzo: Getty Images

Jengo la ghorofa 52, mojawapo ya majengo marefu zaidi katika eneo hilo na makazi ya zaidi ya wakaazi 1,500 wa mataifa mbalimbali, linajulikana sana kwa kuwahifadhi Wakenya wengi wanaofanya kazi UAE.

Kwa mujibu wa Khaleej Times, moja ya vyombo vya habari nchini UAE, Mkenya huyo aliyefahamika kwa herufi za mwanzo B.K. aliripotiwa kujaribu kujiokoa kutoka kwa jengo hilo kwa kushuka kwa kutumia nyaya zilizoko nje ya ghorofa.

Rafiki wa karibu na mpangaji mwenzake, Aby, alisema kuwa huenda B.K. alipoteza usawa na kuanguka hadi kufa.

?Labda alidhani hiyo ndiyo njia pekee ya kutoka. Huenda aliona nyaya nje ya dirisha na akaamini anaweza kushuka kuzitumia? lakini lazima aliteleza na kuanguka,? Aby alisema.

Aby, ambaye alinusurika katika moto huo, alikumbuka jinsi B.K. alivyofanya juhudi za kishujaa kabla ya mkasa huo.

Alisema B.K. ndiye aliyekuwa wa kwanza kugundua moshi mzito mweusi ukiingia kwenye nyumba yao katika jengo hilo la ghorofa 52.

?Ilikuwa ni mwisho wa wiki, wengi wetu tulikuwa bado tumelala moshi ulipoanza kuingia kwenye chumba chetu. Nilichosikia tu ni B.K. akipiga kelele akituamsha na kutuambia tutoke nje,? alisema.

Aliongeza kuwa hali ya taharuki ilitanda haraka moshi ulipozidi, lakini B.K. alibaki mtulivu, akiwashauri wenzake kufunika nyuso zao ili kuepuka kukosa hewa.

Wakati Aby na wengine waliokolewa na kikosi cha uokoaji cha ulinzi wa raia, B.K. hakuonekana tena.

?Tulijua kilichotokea baada ya kuokolewa. Kulikuwa na vurugu nje ? polisi, wazima moto, watu kila mahali. Nikasikia mtu alikuwa ameruka, na baadaye mpangaji mwingine alithibitisha kuwa alikuwa ni B.K. Sote tulipatwa na mshtuko. Yeye ndiye aliyetuhakikishia tutoke salama kwa wakati.?

Aby, kwa machozi, alimwelezea B.K. kama mchangamfu na mcheshi. B.K. alikuwa akifanya kazi katika duka kubwa la biashara (mall) na alikuwa amehamia katika jengo hilo hivi karibuni ili kupunguza gharama ya kodi.

?Bado siamini kwamba ametuacha,? Aby alisema.

Je, watu wengine wanne walikufaje kwenye moto huo?

Inaripotiwa kuwa waathiriwa wanne walianguka wakijaribu kukimbia moto huo, huku mwingine akiaminika kufariki kutokana na mshtuko wa moyo, huenda kwa sababu ya hofu.

Mmoja wa wahasiriwa wawili wasiotambulika ? anayesadikiwa kuwa Mkenya anayeitwa kwa jina moja ? aliteketea hadi kutotambulika, jambo linafanya ie vigumu kimtambua.

Mamlaka bado haijabaini chanzo cha moto huo. Polisi wa Sharjah wamesema uchunguzi unaendelea.

Kwa mujibu wa polisi, moto ulianzia katika moja ya ghorofa za juu, na kusababisha uokoaji wa haraka wa mamia ya wakaazi.

Read ENGLISH VERSION

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia [email protected] au WhatsApp: 0732482690.

Chanzo: TUKO.co.ke