Trans Nzoia: George Natembeya Apuuza Madai ya Ukabila, Anaapa Kufanya Maendeleo Licha ya Changamoto

Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya amepuuzilia mbali madai ya ukabila akiyahusisha na vitisho vya kisiasa kabla ya 2027

Natembeya alielezea miradi kadhaa mikubwa inayoendelea, ikiwa ni pamoja na hospitali ya kisasa ya uzazi na uwanja wa michezo wa viti 20,000

Alithibitisha dhamira yake ya kutoa huduma licha ya shinikizo la kisiasa na changamoto zinazoendelea katika sekta ya afya

Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya anasema anaandamwa na mashambulizi yaliyoratibiwa ya kisiasa yanayolenga kuvuruga ajenda yake ya uongozi na maendeleo.

George Natembeya amewakemea wakosoaji wake akidai kuwa hawana amani kutokana na ushawishi wake. Picha: George Natembeya.

Chanzo: Facebook

Haya yanajiri kufuatia matamshi ya Seneta wa Nandi, Samson Cherargei, ambaye alidokeza uwezekano wa hoja ya kumng?atua madarakani Gavana Natembeya, ikiongozwa na wafuasi wa serikali.

Kwa mujibu wa Cherargei, matamshi ya Natembeya yanaweza kuchochea migawanyiko ya kikabila katika kaunti ya Trans Nzoia ambayo ina watu kutoka makabila mbalimbali.

Hata hivyo, Natembeya amekanusha vikali madai hayo, akieleza kuwa msimamo wake thabiti kuhusu siasa za eneo hilo na maendeleo jumuishi umeleta wasiwasi kwa watu waliokuwa wakinufaika kutokana na mgawanyiko wa muda mrefu katika eneo hilo.

Anasema hali hiyo ya kisiasa imezua hofu kuhusu ushawishi wake na wa eneo hilo katika siasa za kitaifa za mwaka 2027.

"Ilichukua mtu mmoja tu kubadilisha mwelekeo wa siasa za eneo hili. Alipofariki, watu wengi walianza kulidharau eneo hili. Ndiyo sababu tunasema lazima tujikusanye tena," alisema Natembeya.

Je, Natembeya ana rekodi gani ya utendakazi Trans Nzoia?

Natembeya pia amepuuza madai kuwa serikali yake imeshindwa kutekeleza miradi ya maendeleo katika Kaunti ya Trans Nzoia.

"Watu wanahitaji kuelewa jinsi serikali hufanya kazi. Tulipoingia ofisini, tulikagua miradi yote iliyopendekezwa. Baadhi tayari zilikuwa na michoro ya awali, tukalazimika kutafuta marafiki wa kushirikiana nao. Baadhi ya miradi hii iko karibu kukamilika," aliongeza.

Gavana huyo mashuhuri alieleza miradi kadhaa ya maendeleo ambayo anaamini itabadilisha maisha ya wakaazi wa Trans Nzoia na ukanda mzima wa Magharibi pindi itakapokamilika:

1. Hospitali ya Akina Mama na Watoto ya Tom Mboya

Natembeya alitaja kituo hiki kama kipaumbele kikuu cha serikali yake. Mara kikikamilika, kitakidhi mahitaji yanayoongezeka ya huduma za afya kwa akina mama na watoto katika kaunti.

"Kituo hiki cha kisasa kitahudumia kina mama na watoto wetu. Ni cha kipekee, nawahakikishia wakazi," alisema.

2. Uwanja wa Michezo wa Kenyatta

Natembeya alikumbusha kuwa ajenda ya vijana ilikuwa sehemu ya ilani yake ya kampeni, ambayo ilimsaidia kupata kiti cha ugavana.

Kwa mujibu wake, uwanja huu utawapa vijana miundomsingi ya kukuza vipaji vyao na kuwapa fursa ya kujulikana kimataifa.

"Uwanja huu utakuwa na uwezo wa kuchukua watu 20,000. Utakuwa wa matumizi mengi, ukiwa na ofisi, hoteli, na taa za nguvu zitakazowezesha vijana kuutumia ipasavyo na pia kuingizia kaunti mapato," alieleza.

3. Makao Makuu ya Utawala wa Kaunti

Natembeya alielezea mradi huu wa jengo la utawala kama jitihada kabambe, akiongeza kuwa utaleta pamoja huduma zote za serikali ya kaunti na hivyo kupunguza upotevu wa muda na kuboresha utoaji wa huduma kwa wakazi.

"Mradi huu utapunguza upotevu wa muda na kuleta huduma zote za kaunti karibu na wananchi. Utaimarisha usimamizi wa huduma na kudhibiti ufisadi kwa kuhakikisha uwazi kwa kuwa na kituo kimoja cha huduma," alifafanua.

Natembeya alisema nini kuhusu Hospitali ya Rufaa ya Wamalwa Kijana?

Natembeya alikiri changamoto zilizopo katika sekta ya afya katika kaunti yake. Alibainisha kuwa afya ni jukumu la pamoja kati ya serikali ya kitaifa na serikali ya kaunti.

"Hospitali ya Wamalwa Kijana ilikuwa mradi ulioanzishwa na mtangulizi wangu. Tulipochukua hatamu, tuligundua kuwa fedha tayari zilikuwa zimetumika. Tuliteua tume kuchunguza na kupendekeza njia ya kusonga mbele. Tulikuwa na changamoto ya usambazaji wa dawa, lakini sasa tuna dawa za kutosha. Wanasiasa wasiwadanganye wananchi wetu. Hili ni jukumu la pamoja, na tunalishughulikia," alisema.

Read ENGLISH VERSION

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia [email protected] au WhatsApp: 0732482690.

Chanzo: TUKO.co.ke