Kasarani: Wanaume 2 Waliojifanya Wanawake na Kumpora Mteja wa Masaji KSh 280k Wanaswa

Mnamo Alhamisi, DCI ilitangaza kukamatwa kwa washukiwa wawili waliodaiwa kumuibia mwanamume KSh 280,000 Kasarani

Idara ya DCI ilisema kuwa washukiwa hao, wote wawili walikuwa wakijifanya wataalam wa kufanya masaji ili kuwarubuni wateja ambao walikuwa wakitafuta huduma ya kukandwa

Polisi walisema wawili hao, ambao wanafanya kazi kwenye Hifadhi ya Lumumba hawakuwa na ujuzi wowote wa masaji lakini walikuwa wakitangaza huduma zao mtandaoni

Nairobi - Maafisa wa upelelezi kutoka Kituo cha Polisi cha Kasarani wamewakamata wanaume wawili ambao walizua njama ya mtandaoni kuwaibia Wakenya.

Kasarani: Wanaume 2 Wakamatwa kwa Kumtapeli Mteja Aliyetaka Kufanyiwa Masaji KSh 280k

Chanzo: UGC

Katika taarifa iliyotolewa siku ya Alhamisi, Aprili 17, Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) ilisema washukiwa waliotambuliwa kama Alex Mugo Wachira na Simon Chomba Mbogo walikuwa wanajifanya kuwa wanawake waliokuwa wakitoa huduma za masaji.

Kulingana na DCI, wawili hao walikuwa wakivutia wateja kwa kutangaza huduma za kitaalamu za masaji mtandaoni, lakini waligeuka dhidi ya wateja hao wakati wa kikao.

"Maafisa wa upelelezi kutoka Kasarani wamewatia mbaroni wanaume wawili waliokuwa wakifanya utapeli wa mtandaoni kwa kujifanya wanawake warembo wanaotoa huduma za kitaalamu za masaji, lakini badala yake walikuwa wakichukua mali za wateja wao kwa nguvu," taarifa ya DCI ilisema.

Katika mojawapo ya kesi zinazochunguzwa, mwathiriwa mmoja alidanganywa na kile kilichoonekana kuwa wanawake wawili warembo waliotoa huduma za kiwango cha juu za masaji.

Hata hivyo, alipoenda kwenye makazi yanayodaiwa kuwa spa eneo la Lumumba Drive, Kasarani, washukiwa hao wawili walitoa visu na kumtishia.

Kulingana na DCI, wawili hao walimlazimisha mwathiriwa kuhamisha KSh 280,000 kwa nambari yao ya simu, wakampora mali nyingine kisha wakamtupa nje bila huruma.

"Mwathiriwa mmoja, labda akiwa na ndoto za mafuta yenye harufu nzuri na muziki wa spa, aliripoti mkasa huo katika Kituo cha Polisi cha Kasarani. Akiwa amevutiwa na kile kilichoonekana kuwa wanawake wawili warembo waliotoa huduma za masaji ya hali ya juu, alielekea kwenye makazi hayo yaliyoko Kasarani.

"Wawili hao walitoa visu na kufichua utambulisho wao halisi pamoja na kukosekana kwa ujuzi wowote wa masaji. Chini ya tishio, mwathiriwa alilazimishwa kuhamisha KSh 280,000 kwa nambari ya simu ya washukiwa, akapokonywa mali zake kisha kutupwa nje bila huruma,? ilisomeka taarifa hiyo.

Kupitia uchunguzi wa kielektroniki, wawili hao walifuatiliwa hadi eneo la gereza la Kamiti, ambako walikamatwa wakiwa wanajivinjari, huenda kwa kutumia pesa walizoiba.

Mengi kufuata...

Read ENGLISH VERSION

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia [email protected] au WhatsApp: 0732482690.

Chanzo: TUKO.co.ke