Lofa wa Busia Ajinyakulia Ushindi wa Kula Baada ya Kufyeka Chapati 25 kwa Wakati Mmoja

Godfrey Okumu alimshinda mwenzake Henry Otieno katika shindano la kula chapati mjini Busia

Mafundi hao walikaa wakitazamana, wakizingirwa na wenyeji waliokuwa wakishangilia, na Okumu alishinda baada ya kula chapati 25

Walioshuhudia tukio hilo walimwita mfalme wa chapati na wengine wakamtaka Rais Ruto kuleta mashine ya kutengenezea chapati Busia

Katika kile ambacho wengi sasa wanakiita onyesho dhahania la uchu na utayari, makanika wawili kutoka Kaunti ya Busia walijitosa katika shindano lisilo la kawaida lakini la kusisimua la ulaji chapati ambalo limewaacha wenyeji wakiwa wameduwaa na kufurahishwa kwa usawa.

Henry Otieno (l) na Godfrey Okumu (r) katika shindano la kula chapati. Picha: KBC.

Chanzo: Instagram

Tukio hilo, lililorekodiwa na Shirika la Utangazaji la Kenya (KBC), lilimkutanisha Godfrey Okumu na Henrey Otieno walioketi meza moja iliyopambwa kwa chapati, mikate na chupa za soda.

Mfalme wa Chapati wa Busia alitawazwa vipi?

Umati mkubwa wa watu ulikusanyika kuangalia ni nani ambaye angeibuka na taji lisilo rasmi la mfalme wa chapati wa Busia.

Kwa kanuni rahisi ? kula chapati nyingi kadri uwezavyo katika kikao kimoja ? wawili hao walianza kula kwa bidii, wakimeza chapati moja baada ya nyingine huku umati ukishangilia na kushangaa.

Vicheko, mshangao na msisimko vilitawala anga wakati watazamaji walipotazama washiriki hao wakijitahidi kufikia mwisho wao wa uwezo.

Kadri mashindano yalivyopamba moto, ilionekana wazi kuwa Okumu alikuwa na ujuzi wa hali ya juu. Kasi na uthabiti wake vilimlemea Otieno, na baada ya kumaliza chapati 25, Okumu alitangazwa mshindi asiye na mashindano, akishangiliwa kwa heshima na mshangao.

"Sijawahi kuona kitu kama hiki," shahidi mmoja aliambia KBC.

"Mimi nikila chapati tatu, lazima nilale." Mwingine alimwita Okumu kwa urahisi tu, "mfalme."

Cha kufurahisha, hamasa hiyo ya kula chapati imesababisha ombi la kimzaha kutoka kwa wakazi: wanataka Rais William Ruto alete mashine maarufu ya kutengeneza chapati Busia, wakisema kwa utani kuwa ingepata makazi bora zaidi katika kaunti inayopenda chapati kwa dhati.

Wakenya wavunjika mbavu mtandaoni

Wakenya hawakukosa kuchangia furaha hiyo mtandaoni, wakijaza sehemu za maoni kwa vichekesho:

@dickensojiambo275:

"Aina ya habari unazoweza kusikia kutoka Busia."

@tonitodd1922:

"Ile mashine ya chapo ina kazi."

@alextercisio:

"Ukiwa maskini, unaweza fanya kitu chochote."

@mohamedabdullahi9279:

"Anakula chapati 25 na bado ni mwembamba hivi?"

@peternjenga2334:

"Hicho ndicho kitu pekee alichofanyia kaunti yake."

George Natembeya ashuhudia mashindano ya kula

Katika taarifa nyingine, Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya alikuwa mgeni rasmi katika Shule ya Msingi ya Chepchoina, alipolizindua Kombe la Gavana kwa kishindo.

Miongoni mwa shughuli za michezo, shindano la kula liliibuka kama kivutio kikuu, likiwaweka wakazi katika pambano la kumaliza mkate mkubwa na soda ya lita 2.

Ingawa wengi walikata tamaa njiani, mwanaume mmoja na mwanamke mmoja walikamilisha sehemu zao kwa muda uliowekwa, na kila mmoja alijinyakulia zawadi ya pesa taslimu KSh 2,000, iliyotolewa na gavana mwenyewe.

Mshindi wa Tanzania afyeka chakula kwa dakika 8

Wakati huo huo, ng?ambo ya mpaka nchini Tanzania, mashindano yalikuwa makali vilevile.

Huko Morogoro, washiriki watano walishiriki katika shindano la Tonge Nyama ? shindano la kula lililovutia umati wa watu.

Aliyeibuka kidedea alikuwa David Shauti, aliyekamilisha kula kilo 2 za nyama na wali, na kunywa lita moja ya maji ? yote haya ndani ya dakika nane tu.

Ushindi wake ulimpatia TSh 100,000 (sawa na KSh 5,000) na makofi ya kishindo kutoka kwa watazamaji waliostaajabu.

Read ENGLISH VERSION

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia [email protected] au WhatsApp: 0732482690.

Chanzo: TUKO.co.ke