Aliyekuwa Naibu Gavana wa Vihiga Caleb Amaswache Sasa Anauza Kuni Baada Ya Kuondoka Ofisini

Caleb Amaswache ameingilia uchuuzi wa kuni huko Luanda, kaunti ya Vihiga, ili kujikimu na kulipa bili zake

Aliyekuwa naibu gavana wa kaunti ya Vihiga aliomba nafasi ya kazi kutoka kwa Rais William Ruto

Alisema ana mtoto wa kike anayehitaji ada ya shule, na pia anahitaji mtaji kwa ajili ya biashara yake

Aliyekuwa naibu gavana wa Vihiga Caleb Amaswache amepata chanzo kingine cha riziki baada ya kuacha ofisi yake ya kifahari.

Caleb Amaswache akiwa DG (l) kabla ya kuwa mchuuzi wa kuni (r). Picha: mwananchi.digital.

Chanzo: UGC

Baada ya ajira yake ya serikali kumalizika, mtumishi wa zamani wa umma aligeukia kuuza kuni ili kujikimu kimaisha na kulipa bili zake.

Amaswache alieleza kuwa maisha hayakuwa rahisi baada ya kutamatisha kazi ofisini, kwani alipambana sana kuendesha maisha.

Amaswache amuomba Ruto kazi

Amaswache, ambaye ana familia inayomtegemea, alisema kuwa mzigo wa kuwatunza ni mkubwa mno.

"Nahitaji kazi. Namwomba Mheshimiwa Rais William Ruto awazingatie waliowahi kuhudumu serikalini. Sisi sote ni Wakenya, na rais anapaswa kutujali sisi wote," alisema kwa huzuni kubwa alipokuwa akizungumza na Citizen Digital.

Amaswache, aliyewahi kufanya kazi chini ya aliyekuwa gavana wa Vihiga, Moses Akaranga, alisema kuwa anahitaji angalau KSh 200,000 kama mtaji.

Nyumbani, kumbukumbu pekee alizonazo za viongozi wa serikali aliowahi kufanya nao kazi ni picha zilizowekwa kwenye fremu.

Ushauri wa Amaswache kwa wanasiasa

Mzee huyo aliyejaa machungu aliwaonya viongozi wa sasa dhidi ya kuwadharau waliowatangulia ofisini.

"Walindeni na waheshimuni waliowahi kuhudumu katika ofisi. Leo uko ofisini, kesho hujui," alisema kwa uchungu.

Alisema kuwa mtu akiwa madarakani kila kitu huonekana kizuri na anaheshimiwa kwa sababu ya nafasi yake.

"Lakini ukiwa nje ya mamlaka, ndipo unapogundua hali halisi ya mambo. Watu hawatashika simu zako kwa sababu hawakuhitaji tena," aliongeza.

Wakenya watoa hisia mseto kuhusu mabadiliko ya kazi ya Amaswache

Lipesa Victor:

"Inauma kumuona katika hali hiyo. Alikuwa mtu mzuri sana. Alipokuwa Naibu Gavana, alisaidia familia yangu sana tulipopoteza baba kwa saratani mwaka 2014. Alileta pamoja viongozi waliotusaidia kwa harambee kulipa bili ya KSh 3.9 milioni Aga Khan Hospital. Nina deni kubwa kwake. Kwa sasa, ninaweza tu kuomba. Mungu akitujalia, nitamlipa kwa wema wake."

Raduku Oketch:

"Kuwa na vyeo kama 'naibu' ambavyo havina majukumu bayana na kutegemea mabosi wako ni hali tata. Inasikitisha kwa wanaoshikilia nyadhifa kama hizi kwa sasa. Jambo jema ni kwamba hawatafikishwa mahakamani kwa masuala ya ufisadi."

Walter James:

"Lakini vipi sasa? Tuseme labda aliishi kwa uwezo wake? Hata hivyo, inawezekanaje hana uwekezaji wowote? Inaonekana sasa ameelewa kwamba mamlaka ni ya muda, lakini je, alijua hivyo alipokuwa madarakani? Simlaumu wala simhukumu, ni udadisi tu unaniongoza kama paka."

John Oletito:

"Elimu ya kifedha ni somo la kila siku. Hadithi hii inaonyesha umuhimu wa kuwa na ujuzi wa kifedha katika kusimamia kipato. Kuwa na mshahara wa milioni bila kuwekeza kunaweza kusababisha aibu baadaye. Wakati mwanaume yuko chini, usimchekelee."

Wekesa Brown:

"Na hii ndiyo sababu baadhi ya jamaa zetu huwa wabahili. Labda huyu jamaa alikuwa mkarimu kupita kiasi, alisomesha watoto, alilipia matibabu, sasa hivi ni gumzo la kudharauliwa. Watu wanapaswa kuelewa si kila mtu huweka thamani ya pesa kuliko utu. Ningependa kusaidia watu hata kama inamaanisha kufa maskini. Usimhukumu mtu kama huyu. Hujui historia yake. Furahia maisha, na saidia kupunguza huzuni za wengine ? hiyo ndiyo maana halisi ya maisha."

Aliyekuwa Gavana wa Vihiga Moses Akaranga alifanya kazi na Caleb Amaswache. Picha: Mkenya Mjerumani.

Chanzo: UGC

Chipukeezy apata kazi nono katika ofisi ya Ruto

Wakati huohuo, mchekeshaji maarufu Chipukeezy aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Itifaki katika Ofisi ya Rais.

Uteuzi huo ulitangazwa na Dennis Itumbi, anayehudumu kama Mkuu wa Miradi Maalum ya Rais na Uchumi wa Ubunifu.

Read ENGLISH VERSION

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia [email protected] au WhatsApp: 0732482690.

Chanzo: TUKO.co.ke